Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

WAWEKEZAJI KUTOKA INDIA WAPONGEZA MAZINGIRA YA UWEKEZAJI NCHINI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, Novemba 23, 2023 jijini Dodoma amekutana na kufanya mazungumzo na wawekezaji kutoka nchini India ambao wameonesha nia ya kuweza katika sekta za kilimo na miundombinu.

Akizungumza na wawekezaji hao, Prof. Mkumbo amesema kuwa Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali za  kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.

“Ujio wa wawekezaji hawa wenye nia ya kuwekeza katika mashamba ya miwa na kiwanda cha sukari ni matunda ya ziara ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini India aliyofanya mwezi Oktoba mwaka huu, hivyo Serikali inaendelea na jitihada mbalimbali ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi”, Amesema Prof. Mkumbo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya DHD Infracon Pvt Ltd kutoka nchini India, Bw.  Subhash Landade amesema kuwa wamevutiwa kuja kuwekeza nchini kwa sababu ya mazingira bora ya uwekezaji.

“Nimetembelea  nchi nyingi za Afrika lakini tofauti ya Tanzania na nchi nyingine ni uwepo wa utulivu wa kisiasa, ardhi yenye rutuba  na upatikanaji wa maji ya kutosha  haya yote ni mambo ya muhimu kwetu, nia yetu ni kuwekeza Tanzania katika sekta ya kilimo na viwanda hususan katika uzalishaji wa sukari ”, amesema Bw. Subhash.

Ameongeza “Uhusiano wa Tanzania na India umekuwepo kwa miaka mingi na biashara kati yetu zimefanyika kwa muda mrefu hivyo tunajisikia furaha kuwa Tanzania”.

Vilevile, Bw. Subhash ametoa rai kwa wawekezaji kutoka maeneo mengine duniani kuja kuwekeza nchini kwa kuwa kuna malighafi za aina mbalimbali ambazo zinaweza kuwafaa katika uwekezaji wao.