Habari
WAZIRI MKUU ATOA MAONI KUHUSU DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb,), ametoa maoni kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo alipokutana na Mwenyekiti wa Timu ya Uandishi wa Dira, akiambatana na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Nyongo.
Mheshimiwa Majaliwa alisisitiza umuhimu wa Dira hiyo kwa kusema, “Dira hii itatusaidia kuwa na mipango ya miaka mitano mitano, na hatimaye serikali kuwa na mpango wa mwaka hadi mwaka ambao utasaidia katika kupanga bajeti ya serikali kwa ujumla.”
Aliongeza kuwa Dira ya Taifa lazima izingatie tunu muhimu za taifa kama usalama wa nchi, amani, na mshikamano, ambavyo ni msingi wa mafanikio ya taifa letu. Pia, alisisitiza umuhimu wa utawala bora kuanzia ngazi ya vijiji hadi kitaifa ili kujenga taifa endelevu lenye jamii iliyoelimika na inayofundishika.
Kwa upande wa uchumi, Mheshimiwa Majaliwa alieleza kuwa Dira hiyo inalenga kujenga jamii yenye uchumi binafsi, ambapo kila Mtanzania ataweza kujipatia kipato kupitia rasilimali za nchi kama ardhi, mito, na bahari, na hivyo kuchangia katika kukuza uchumi wa taifa.
Katika hotuba yake, alitoa wito kwa jamii kuelewa mabadiliko ya tabianchi na kuwa tayari kukabiliana nayo. Aidha, alisisitiza ushiriki wa wanawake katika shughuli za kujenga taifa, akisema kuwa Dira hiyo inapaswa kubadili mifumo ya kijamii inayodumaza nafasi za wanawake, na kuainisha fursa zinazoweza kumuinua mwanamke nchini.