Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

Programu na Miradi zaidi ya 100 kutekelezwa mwaka wa fedha 2024/2025.


Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof.Kitila Mkumbo wakati akiwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2024/2025, miradi na programu 162 zitatekelezwa ili kuchochea kasi ya ukuaji uchumi unaopunguza umaskini na kuleta ustawi kwa wote.

Akiwasilisha leo mapendekezo ya serikali ya mpango huo kwenye mkutano wa wabunge, Prof. Mkumbo, amesema lengo la mpango huo ni kuzalisha ajira kwa wingi na kuchochea mauzo ya bidhaa zilizoongezwa thamani nje ya nchi.

Prof.Kitila amesema katika kuchochea, programu na miradi 162 itatekelezwa ambayo ni miradi ya kielelezo, ikiwemo mradi wa reli ya kisasa ya SGR na miradi ya kufua nishati ya umeme kama vile bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere, Ruhudji, Rusumo, Rumakali, Kinyerezi, na miradi ya umeme wa jua na upepo.

Pia amesema kuendelea kupanua na kuimarisha miundombinu ya usafiri wa barabara, reli, anga, na majini, na utunzaji endelevu wa mazingira na nchi inaimarisha matumizi ya gesi (CNG) katika uendeshaji wa magari ili kuanza kupunguza utegemezi wa mafuta ya kuagiza nje ya nchi.

Kadhalika, amesema  kuimarisha huduma za ugani, kupanua kilimo cha umwagiliaji, ikiwemo kukamilisha skimu 25, kukarabati skimu 30 na kukamilisha ujenzi wa mabwawa 14 ya kuvuna maji ya mvua, kuimarisha upatikanaji wa pembejeo kwa wakulima, ikiwemo kununua magari matano yenye uwezo wa kubeba tani 30 za mbegu, kujenga maabara mbili za mbegu, kununua vifaa vya utafiti na kujenga maghala matatu ya kuhifadhia mbegu.

“Kuendelea kutekeleza programu ya BBT kwa kutambua na kuanisha mashamba mapya 30 katika mikoa mitano, kupima ardhi ya kilimo kwa ajili ya uwekezaji katika mikoa kumi, kutoa mafunzo kwa walengwa 1000, kutoa mikopo ya riba nafuu kwa vijana na wanawake na kuhamasisha uanzishwaji wa kampuni za ugani kwa kushirikisha vijana wanaohitimu mafunzo ya kilimo,”amesema.

Pia, alisema kuweka mazingira maalum katika kuvutia ujenzi wa viwanda vidogo vijijini kwa lengo la kufanya ongezeko la awali la thamani (primary processing) katika sekta za kimkakati, zikiwemo kilimo, mifugo, uvuvi, na misitu.

“Serikali itatumia sera za kifedha na kikodi ili kuvutia wawekezaji katika maeneo ya vijijini ili mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na misitu yatoke vijijini yakiwa yameanza kufanyiwa uchakataji wa awali (semi-processed).”

“Viwanda vya vijijini vitabakisha thamani kubwa kijijini na kutoa nafasi ya ajira kwa vijana na wanawake ambao wengi wao sasa wana elimu ya sekondari. Kuendelea kuhamasisha, kutangaza na kuwezesha uwekezaji, kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi,”alisema.

Pamoja na hayo, alisema kupitia upya mfumo wa kodi ili kuweka mazingira ya kukua kwa wigo wa walipa kodi sambamba na ukuaji wa pato la taifa, kufanya tathmini ya mahitaji ya raslimali watu, kuzingatia umuhimu wa dijitalikatika kuleta mapinduzi ya uchumi vijijini.

“Serikali itaanzisha mradi wa kujenga mfumo wa dijitali vijijini ili kuwaunganisha wananchi vijijini katika uchumi wa taifa na kuongeza matumizi ya TEHAMA katika shughuli za kiuchumi na kijamii,”amesema.

Waziri Mkumbo amesema kwa kuzingatia nafasi ya madini katika kuendelea kukuza ujazo wa mauzo ya nje, serikali itaweka mazingira mahususi kwa lengo la kuvutia wawekezaji watakaokuwa tayari kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya madini hapa nchini, hususani katika ujenzi wa viwanda vya kuzalisha betri za magari na mitambo.

Prof.Mkumbo alisema katika kuchochea maendeleo ya watu na ustawi wa jamii, programu na miradi 62 itatekelezwa ikiwamo kuendelea na upanuzi na uboreshaji wa miundombinu ya kutolea huduma za afya, pamoja na upatikanaji wa vifaa tiba.

“Kuendelea kutekeleza miradi ya usambazaji maji na usafi wa mazingira, ikiwamo kuendelea na maandalizi ya kutekeleza mradi wa kusafirisha maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Singida na Dodoma kwa ajili ya maji safi ya kunywa na umwagiliaji,”amesema.

Amebainisha kuendelea na upanuzi na uboreshaji wa miundombinu ya kujifunza na kujifunzia, pamoja na upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika ngazi zote za elimu.

“Kuendelea na utekelezaji wa programu ya kutoa elimu ya msingi na sekondari bila ada, kutoa mikopo kwa wanafunzi 93,500 wa elimu ya juu na elimu ya kati, wakiwemo wanafunzi 10,000 wa mafunzo ya stashahada, kutekeleza sera na mitaala mipya ya elimu, ikiwemo mafunzo kwa walimu,” amesema.