Habari
DIRA 2025 ITUMIKE KAMA MSINGI WA DIRA 2050 – PROF. KITILA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amewahimiza wafanyabiashara kutambua mchango wa Dira ya Taifa 2025 kwa kuyaenzi mambo mazuri yaliyopatikana kupitia Dira hiyo ili kujenga msingi wa Mipango ya Dira ya 2050.
Mhe. Prof. Mkumbo ametoa wito huo wakati akizungumza katika Mkutano baina ya wafanyabiashara na wamiliki wa kampunu na Timu Kuu ya Uandishi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 jijini Dar es Salaam, leo Januari 8, 2025, ambapo amesistiza kuwa mafanikio yaliyopatikana kutoka Dira ya 2000-2025 ni hazina muhimu kwa maendeleo ya miaka 25 ijayo.
“Mambo tuliyoyafanya kwa uzuri yanapaswa kuwa msingi wa Dira 2050. Hata hivyo, ni muhimu pia kuachana na yale ambayo hayakuwa na matokeo chanya katika kipindi kilichopita,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Mhe. Waziri aliwataka wafanyabiashara kushiriki kikamilifu katika kukuza Pato la Taifa na la mtu mmoja mmoja, akiwasihi kutumia ujuzi wao wa kitaaluma katika kuibua fursa mpya na kushughulikia changamoto zilizopo.
Mkutano huo umewaleta pamoja wadau mbalimbali wa sekta ya biashara kwa lengo la kuimarisha Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kwa kuzingatia masuala ya msingi yanayochangia ustawi wa uchumi na maendeleo ya jamii.