Habari
DKT. BITEKO ATOA WITO KWA WANANCHI KUTOA MAONI KUHUSU DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Dotto Mashaka Biteko (Mb.), ametoa wito kwa wananchi kutoa maoni kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili dira inayoandikwa iweze kuakisi maono ya kitaifa.
Dkt. Biteko ametoa wito huo leo jijini Mwanza alipozindua rasmi Kongamano la kwanza a Kikanda la Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambapo amewasihi washiriki kutumia fursa ya jukwaa hilo kujiuliza maswali yatakayoijenga Tanzania waitakayo miaka 25 ijayo.
“….tujiulize tulikotoka kama nchi, tuko wapi? Mambo yapi yanayotokea ulimwenguni na yanatuathiri vipi? tunataka kuelelekea wapi na tunafikaje huko?....” amechagiza mjadala Mhe. Dkt. Biteko.
Aidha, Naibu Waziri Mkuu, amezitaja changamoto zilizopo ulimwenguni na namna zinavyoweza kuathiri maendeleo ya nchi, ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi, tekinolojia, demografia, mpasuko wa kisiasa wa dunia na kukosekana kwa utulivu wa kijamii akiwasihi washiriki wa kongamano hilo kutafakari namna ya kukabiliana changamoyo hizo.
“Changamoto hizo zinaathari za moja kwa moja, kwa mfano mabadiliko ya tabianchi yamesababisha mitaji na uwekezaji mwingi kuelekezwa katika miradi ya kuzalisha nishati safi, hivyo tunalazimika kubadilika kwenda uelekeo huo” Amesema Dkt. Biteko.