Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

DKT. KIDA AKAGUA UJENZI WA JENGO LA OR - MU MTUMBA, ATOA MAELEKEZO YA KUHARAKISHA MRADI


Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji (OR-MU), Dkt. Taus Kida, ameongoza timu ya menejimenti ya Ofisi hiyo kukagua ujenzi wa jengo jipya la Ofisi yake katika Mji wa Serikali Mtumba, ambapo ameelekeza mkandarasi wa mradi huo, Suma JKT, kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati ili kuwezesha watumishi kuhamia katika ofisi hizo mapema.

Ziara hiyo iliyofanyika leo, Januari 16, 2025, ililenga kutathmini maendeleo ya mradi huo ambao kwa sasa umefikia asilimia 64 ya utekelezaji wake.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Dkt. Kida alieleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi pamoja na ubora wa kazi, lakini alisisitiza mkandarasi kuongeza kasi kwenye maeneo yaliyo nyuma ili kufanikisha kukamilika kwa mradi huo ndani ya kipindi cha miezi sita kama ilivyopangwa.

“Lazima tuhakikishe maeneo yaliyoko nyuma yanafanyiwa kazi kwa kasi kubwa ili kufikia malengo kwa mujibu wa mpango kazi uliopo,” alisema Dkt. Kida huku akimpongeza mkandarasi kwa hatua kubwa iliyofikiwa.

Pia alisisitiza kuwa kukamilika kwa jengo hilo kutaimarisha mazingira ya kazi kwa watumishi wa ofisi hiyo na kuchangia katika ufanisi wa utekelezaji wa mipango ya serikali.