Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

DKT. KIDA AKUTANA NA BALOZI WA KOREA KUJADILI MAENDELEO NA UWEKEZAJI


Januari 8, 2025. Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida, amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Korea nchini, Mheshimiwa Ahn Eun Ju, ambapo wamejadili masuala ya mipango ya maendeleo na kuimarisha uwekezaji wa sekta binafsi ya Korea nchini Tanzania.

Katika kikao hicho, Dkt. Kida amemkaribisha Balozi Ahn na kumshukuru kwa mchango wa Korea katika maendeleo ya Tanzania tangu uhusiano wa kidiplomasia ulipoanzishwa mwaka 1992.

Aidha, amebainisha maeneo muhimu ambako Korea, kupitia Shirika lake la Maendeleo (KOICA), imekuwa ikisaidia Tanzania, akitaja sekta za afya, elimu, miundombinu, uchukuzi, na teknolojia.
Wawili hao, wamejadili hatua za kitaalam za kuendeleza mazungumzo kuhusu Mkataba wa Kukuza na Kulinda Uwekezaji (BIT) kati ya nchi hizo mbili katika kikao hicho kilichokuwa na ushiriki wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Kwa upande wake, Balozi Ahn amesisitiza dhamira ya Serikali ya Korea ya kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika nyanja mbalimbali zinazolenga kuboresha ustawi wa mataifa yote mawili.