Habari
SERIKALI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA UNIDO KATIKA UWEKEZAJI WA KONGANI YA VIWANDA NCHINI
Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Sekta Binafsi Bw. Aristides Mbwasi kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Dkt. Tausi Kida ameliomba Shirikia la Maendeleo ya Viwanda la Umoja wa Mataifa (UNIDO) kusaidia kufanya utafiti wa awali katika maeneo ya uwekezaji wa viwanda ili kuiwezesha Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji kuandaa muongozo wa uwekezaji katika maeneo ya viwanda.
Bw. Mbwasi ameyasema hayo leo Oktoba 15,2023 Mkoani Dodoma alipokutana kwa mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Umoja wa Mataifa (UNIDO), Bw. Victor Djemba
Bw. Mbwasi ameongeza kuwa Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji ina jukumu la kuratibu na kuwezesha masuala ya uwekezaji nchini hivyo amekaribisha uanzishwaji wa maeneo ya viwanda.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Umoja wa Mataifa (UNIDO), Bw. Victor Djemba ameeleza utayari wa UNIDO kuendelea na maandalizi ya utekelezaji wa Mpango wa Ushirikiano wa Nchi (Program for Country Partnership-PCP) uliobuniwa na UNIDO kwa ajili ya kutekeleza dhana ya Maendeleo Jumuishi na Endelevu ya Viwanda (Inclusive and Sustainable Industrial Development-ISID).
Bw. Djemba amefafanua kuwa Mpango wa PCP ulibuniwa na UNIDO mwaka 2013 ili kutekeleza lengo la 9 la Maendeleo Endelevu (SDG) la Umoja wa Mataifa linalolenga kuendeleza viwanda, ubunifu na ujenzi wa miundombinu kwa nchi wanachama ifikapo mwaka 2030 ambapo mtekelezaji mkuu wa lengo hilo ni UNIDO kwa kushirikiana na nchi wanachama na wadau wengine. Utekelezaji wa Mfumo wa PCP unatarajiwa kuzinufaisha nchi wanachama wa UNIDO ikiwemo Tanzania.
Aidha, ilibainishwa kuwa katika utekelezaji wake, Serikali itashirikiana na UNIDO na wadau wengine wa maendeleo katika kuandaa mikakati kwa ajili ya upatikanaji wa rasilimali za kutekeleza mfumo PCP na kuainisha maeneo ya kipaumbele ya uchumi wa viwanda kwa kuzingatia Mipango ya Maendeleo ya Nchi na kuandaa utaratibu wa kushirikisha Sekta binafsi katika kutekeleza PCP.