Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

MHE. NYONGO AZITAKA MAMLAKA ZA SERIKALI KATIKA MKOA WA DODOMA KUTUMIA TAARIFA ZILIZOPO KATIKA KITABU CHA PATO LA MKOA NA WASIFU WA UCHUMI


Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Stanslaus Nyongo (Mb) amezitaka Mamlaka za Serikali katika ngazi zote mkoani Dodoma kutumia taarifa zilizopo katika kitabu cha Pato la Mkoa na Wasifu wa Uchumi katika kupanga mipango na programu zao za maendeleo kwa ajili ya kuundeleza Mkoa.

Mhe. Nyongo ameyasema hayo tarehe 5 Novemba 2024 Jijini Dodoma alipokuwa anazindua Kitabu cha Pato la Mkoa na Wasifu wa Kiuchumi na Kijamii wa Mkoa wa Dodoma kinachoelezea Pato la mwananchi mmoja mmoja ngazi ya Wilaya na Mkoa .

Aidha, Mhe. Nyongo ametoa rai kwa Mkoa wa Dodoma kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji na tija katika mazao ya chakula na biashara kwa kuwa ripoti iliyotolewa inaonesha sekta ya kilimo imechangia asilimia 40 kwenye Pato la Mkoa .

Aidha, ametka wito kwa wakuu wa mikoa mingene nchini wafikirie kuiga ubunifu wa mkoa wa Dodoma kwa kuandaa vitabu vya aina hiyo.

“Mlichofanya Mkoa wa Dodoma ni mfano wa kuigwa, unapokuwa na takwimu sahihi inayoonesha idadi ya watu, kipato cha watu na fursa zilizopo ni nyenzo kubwa inayomsaidia mwekezaji kwenda kuwekeza, haya ni mabpo muhimu sana wanayotaka kufahamu wawekezaji" amesema Mhe. Nyongo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema lengo kuu la kuandaa makadirio ya pato la Mkoa ni kutoa kiashiria muhimu cha kiuchumi kitakachotoa mchago katika kupanga mipango ya maendeleo ya Mkoa.

Aidha, kitasaidia kuweka mkazo katika sekta zinazolegalenga ili kuongeza nguvu kwenye maeneo hayo, kutoa msingi thabiti zaidi wa kufanya maamuzi ya kiuchumi kwa Mkoa, wilaya na sekta binafsi.

Nae Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Albina Chuwa, ameupongeza Mkoa wa Dodoma kwa kutimiza agizo lililotolewa na Waziri Mkuu la kuandaa vitabu vya kitabu cha pato la mkoa na wasifu wa uchumi ili kuvutia wawekezaji nchini, pia ameiomba Tume ya Mipango kuendelea kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya Makatibu Tawala wa mikoa yote nchini ili kuendelea kukusanya takwimu ambazo zitamuwezesha mwekezaji kufahamu maeneo ya kuwekeza.

Vitabu vilivyozinduliwa vimejumuisha taarifa za wilaya zote saba za Mkoa wa Dodoma kwa kuonesha hali ya kiuchumi, kijamii na kidemografia ya Mkoa wa Dodoma.