Habari
PROF. MKUMBO AZINDUA MIRADI YENYE THAMANI YA BILIONI 6.6 IKIHUSISHA KITUO CHA MABASI, KITUO CHA AFYA CHA BOSSOUT NA MIUNDOMBINU YA SHULE YA MULBADAW
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, amezindua miradi yenye thamani ya kiasi cha Shilingi 6,637,059,000 ikusisha ujenzi wa Kituo cha Mabasi cha Katesh, kituo cha afya cha Bossout na miundombinu ya shule ya sekondari ya Mulbadaw.
Mheshimiwa Mkumbo ameeleza umuhimu wa miradi hiyo kwa wananchi wa Mkoa wa Manyara na kutoa maagizo mazito kwa mkandarasi anayejenga Stendi Mpya ya Mabasi ya Katesh kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.
Akizungumza wakati wa kuweka jiwe la msingi la stendi hiyo inayojulikana kama Stendi ya Dkt. Samia Suluhu Hassan wilayani Hanang, Mkoa wa Manyara, Mhe. Mkumbo alisisitiza umuhimu wa mradi huo katika kurahisisha huduma za usafiri na kukuza biashara za wananchi.
Mradi huo una thamani ya Shilingi Bilioni 5.69, ukigharimiwa kikamilifu na Serikali ya Awamu ya Sita.
Waziri Mkumbo alisema kuwa lengo la Serikali ni kuboresha maisha ya wananchi kwa kubuni miradi inayorahisisha upatikanaji wa huduma muhimu.
“Mradi huu mkubwa utawanufaisha akina mama na vijana, ambao wanapaswa kupewa kipaumbele katika nafasi za biashara zitakazotokana na stendi hii,” aliongeza.
Mbunge wa Jimbo la Hanang, Mhandisi Samwel Hhayuma, alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutatua changamoto kubwa za jamii, ikiwemo maji, afya, elimu, na miundombinu ya barabara.
Alisema maendeleo yanayoonekana sasa ni matokeo ya juhudi thabiti za Serikali ya Awamu ya Sita.
Stendi hiyo mpya inajengwa kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 5.88, na kazi inatekelezwa na mkandarasi mzawa, Elerai Construction Company Limited, huku usimamizi wa kitaalamu ukifanywa na Bureau for Industrial Cooperation (BICO) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hadi sasa, mradi umefikia asilimia 85 ya utekelezaji.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Bi. Teresia A. Irafay, stendi hiyo itakuwa na majengo ya kisasa, ikiwemo jengo lenye ghorofa moja kwa ajili ya abiria kusubiri mabasi, ofisi za utawala, na majengo matatu yenye vyumba 90 vya maduka.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkumbo pia alitembelea Shule ya Sekondari ya Mulbadaw, ambako alizindua mradi wa miundombinu ya maabara za masomo ya sayansi.