Habari
RAIS DKT. SAMIA AVUNJA REKODI YA UWEKEZAJI TANZANIA: MIRADI 901 YAVUTIA MITAJI YA DOLA BILIONI 127
Dar Es Salaam, Januari 10, 2025
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeandika historia kwa kuvutia uwekezaji mkubwa zaidi katika mwaka 2024, ambapo miradi 901 ilisajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Miradi hii imevutia jumla ya mitaji ya Dola za Kimarekani bilioni 127, kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa tangu kuanzishwa kwa TIC.
Waziri wa Nchi, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo ametoa taarifa hiyo leo, Januari 10, 2025, Jijini Dar es Salaam katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari na kusema kuwa mafanikio hayo ni ushahidi wa dhamira thabiti ya Rais Samia katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
"Hii ni miradi mingi zaidi kuwahi kusajiliwa, na Rais Samia ameonyesha maono makubwa tangu ahadi yake aliyoitoa Aprili 2021 alipohutubia Bunge," amesema Warizi Mkumbo.
Mhe. Mkumbo amebainisha kuwa mafanikio hayo pamoja na mambo mengingine yametokana na maboresho makubwa ya kisera na kisheria yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, amabayo ni pamoja na kuimarisha mifumo ya kidijitali, kupunguza urasimu, na kutoa vivutio vya kikodi kwa wawekezaji.
Aidha, juhudi za Rais Samia katika ushawishi wa makampuni makubwa kupitia ziara za kimataifa na mikutano zimeimarisha imani ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Aidha, uanzishwaji wa ofisi mpya ya TIC Kanda ya Kaskazini, mkoani Arusha, umetajwa kuwa kichocheo kikubwa cha uwekezaji kwenye sekta ya utalii ambapo Mhe. Waziri Mkumbo amesifu jitihada za Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, na Mamlaka za mikoa kwa kuhamasisha biashara na uwekezaji katika maeneo yao.
Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeweka alama isiyofutika katika historia ya maendeleo ya Tanzania. Uwekezaji wa mwaka 2024 siyo tu unachochea uchumi wa Taifa, bali pia unatoa matumaini mapya kwa Watanzania kuhusu mustakabali wa maendeleo yao.