Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

Serikali Kufanya utafiti mji wa Tunduma kubaini fursa za kukuza uchumi


Serikali imesema kuwa Tume ya Mipango itafanya tafiti mbalimbali kubaini fursa za maendeleo katika miji ikiwemo Mji wa Tunduma kwa lengo kujua ni jinsi gani mji huu na miji mingine inaweza kuongeza kasi ya maendeleo na kuchangia kukuza uchumi wa nchi.

Hayo yamelelezwa na leo Februari 2, 2024 Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalaum, Mhe.  Neema Mwandabila, aliyeuliza kuhusu mkakati wa Serikali wa kufanya utafiti maalum katika Mji wa Tunduma ili kubaini ni namna gani unaweza kuchangia kukuza uchumi wa nchi.

"Tume ya Mipango imejipanga kufanya tafiti mbalimbali na kuratibu tafiti zitakazofanywa na taasisi nyingine za umma na binafsi kwa lengo la kubaini fursa za maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini. Aidha, kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Mipango, hususani kifungu cha 6(2), pamoja na majukumu mengine, Tume ya Mipango ina jukumu la kufanya utafiti kuhusu suala lolote ambalo Tume inaona ni muhimu katika kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa", ameeleza Prof. Mkumbo.

Vilevile, Prof. Mkumbo amejibu swali la nyongeza la Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Mhe. Angelina Mabula kuhusu utekelezaji wa mradi wa kongano la viwanda lenye ekari 52 lilotengwa katika Manispaa ya Ilemela eneo la Nyamuhoro.

Ambapo, Prof. Mkumbo amesema "Eneo hilo limeshakabidhiwa  katika Taasisi ya EPZA  na linafanyiwa kazi, aidha litawasilishwa  katika Bodi  na baada ya hapo litatolewa maelekezo maalumu ni  lini hasa ratiba itatoka ya utekelezaji na katika Bunge lijalo tutaeleza Mpango maalumu kuhusu kongano hilo".