Habari
SERIKALI YAZINDUA MAANDALIZI YA MPANGO WA PILI WA MABORESHO YA MAZINGIRA YA BIASHARA NA UWEKEZAJI (MKUMBI II)

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amezindua rasmi Mchakato wa Kuandaa Mpango wa Pili wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI II).
Uzinduzi wa maandalizi ya mpango huo unaonesha dhamira ya dhati ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini.
Zoezi la uzinduzi limekwenda sambamba na kukabidhi nyezo kwa kamati maalum itakayorejea mafanikio na changamoto za Mpango wa Kwanza wa Maboresho ya Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI I) na kuandaa MKUMBI II.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, alieleza kuwa uzinduzi huo unathibitisha mambo makuu matatu yenye uzito kwa wadau wa sekta binafsi na Uchumi;
Kwanza, Uongozi Sikivu, Profesa Mkumbo alisisitiza kuwa serikali imesikia na inatambua kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara kuhusu mazingira ya uendeshaji biashara, licha ya kazi kubwa iliyokwishafanyika chini ya MKUMBI I, hatua ya kuanzisha MKUMBI II inaonesha wazi kuwa serikali iko tayari kupokea maoni na kuyatumia kuboresha zaidi.
Pili, Kukabiliana na Mazingira Yanayobadilika, kuhusu mabadiliko ya mifumo ya biashara duniani, Profesa Mkumbo alieleza kuwa MKUMBI II inakuja wakati muafaka ili kuendana na mazingira ya sasa ya kiuchumi, kiteknolojia, na kibiashara. Hii inaashiria uelewa wa serikali juu ya umuhimu wa sera zinazobadilika kulingana na mahitaji ya wakati.
Tatu, Kutafuta suluhuhu ya pamoja: Profesa Mkumbo aligusia uundwaji wa Tume ya Rais ya kushughulikia masuala ya mfumo wa kodi, akieleza kuwa kazi ya kamati hizi mbili (MKUMBI II na Tume ya Kodi) itakapounganishwa, inatarajiwa kutoa mwelekeo madhubuti zaidi katika kuboresha mazingira ya biashara nchini. Hii inaonyesha mtazamo wa kimkakati wa serikali katika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya biashara na uwekezaji kwa ujumla.
Uzinduzi huo wa maandalizi ya MKUMBI II unatoa matumaini mapya kwa wawekezaji na wafanyabiashara nchini kwa kuwa ni ishara ya wazi kuwa serikali inathamini mchango wao katika ukuaji wa uchumi na iko tayari kuweka mazingira wezeshi kwa ustawi wa biashara. Wadau wanatarajia kuona mapendekezo ya msingi na mageuzi ya kweli yatakayotokana na mchakato huu, yatakayoleta tija katika uwekezaji na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu.