Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

TAASISI ZILIZO CHINI YA OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI ZATOA SEMINA KWA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA, UWEKEZAJI WA MITAJI YA UMMA NA BAJETI KUHUSU UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU


Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji leo tarehe 11 Aprili, 2025 imewasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Taifa ya Mipango, Ofisi ya Msajili wa Hazina, Kituo cha Uwekezaji Tanzani (TIC) na Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo Nje (EPZA) kwa kamati ya kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria; Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, pamoja na Kamati ya Bajeti katika ukumbi wa Anna Makinda, Dodoma.

Akizungumza katika semina hiyo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe.Stanslaus Haroon Nyongo (Mb.) kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji amewashukuru waheshimiwa wajumbe wa kamati zote tatu kuitikia wito wa kuhudhuria semina hiyo muhimu yenye lengo la kuwajengea uelewa wa kina  kuhusu majukumu na shughuli za taasisi hizo.

Mhe. Nyongo ameongeza kuwa kamati zote tatu zimekuwa mhimili wa kuboresha utendaji kazi wa Ofisi yake uliopelekea kuongezeka kwa ufanisi wa utendaji katika kuwahudumia watanzania.

“Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru kwa dhati Waheshimiwa wajumbe wote kushiriki katika semina hii muhimu yenye lengo la kujenga uelewa mpana kuhusu majukumu ya taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, ili kusaidia kamati kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kuishauri na kuielekeza Ofisi hii kwa ufanisi zaidi” Amesema Mhe. Nyongo.

Mhe. Nyongo ameeleza mada  zilizoandaliwa ni pamoja na majukumu ya msingi ya kila taasisi husika, shughuli zilizotekelezwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha Awamu ya Sita ya Serikali, changamoto na mikakati ya taasisi kuelekea mwaka wa fedha 2025/2026.

Waheshimiwa Wenyeviti wa kamati zote tatu wamepongeza kazi nzuri inayofanywa na Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji pamoja taasisi zilizo chini yake kwa semina hiyo iliyowajengea uelewa mpana kuhusu utendaji kazi wa Taasisi hizo katika  kuwahudumia watanzania.

Vilevile waheshimiwa wabunge wametoa maoni yao hasa yakilenga kuboresha utendaji kazi wa Ofisi na Taasisi zilizo chini yake na kupongeza Serikali hasa kwa kuja na wazo la kuunganisha Taasisi ya TIC na EPZA na kuundwa kwa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA).