Habari
TANZANIA NA BENKI YA DUNIA KUDUMISHA USHIRIKIANO WA KITAFITI KUIMARISHA KILIMO NA AJIRA

Dodoma, Februari 10, 2025
Serikali ya Tanzania inaendelea be kushirikiana na Benki ya Dunia katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo na ajira.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb.), amekutana na Bi. Rinku Murgai, Meneja wa Kitengo cha Umasikini na Usawa wa Kimataifa, Benki ya Dunia – Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, kujadili ushiriki wa watafiti wa ndani na watunga sera katika tafiti muhimu kwa maendeleo ya taifa.
Tafiti na Ushirikiano wa Kimaendeleo
Prof. Mkumbo amesisitiza kuwa Benki ya Dunia ni mshirika muhimu wa maendeleo nchini, hasa kupitia tafiti zinazotoa mwongozo wa kisera na kusaidia kutatua changamoto za kijamii.
Amesema Serikali inatumia tafiti zinazoratibiwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kuboresha huduma kama upatikanaji wa maji safi, elimu bora, barabara, umeme na miundombinu ya usafiri.
Bi. Rinku Murgai aliambatana na wataalamu wa uchumi, akiwemo Bi. Dhiraji Sharma, Mchumi Mwandamizi wa Masuala ya Umaskini na Usawa wa Kimataifa, pamoja na Bw. Revocatus Washington Paul, mtaalamu wa usawa na umaskini.
Mapitio ya Matumizi ya Rasilimali za Umma Katika Elimu
Katika hatua nyingine, Mhe. Mkumbo amekutana na timu ya wataalamu wa Benki ya Dunia inayoshughulikia tathmini ya matumizi ya rasilimali za umma kwenye sekta ya elimu.
Ripoti ya awali ya tathmini hiyo, inayoongozwa na Dkt. Mari Shojo, imeonesha kuwa Tanzania inafanya vizuri katika utoaji wa elimu ya msingi, sekondari na vyuo vikuu.
Timu hiyo pia inajumuisha Bi. Alasdair Fraser (Mshauri wa Benki ya Dunia) pamoja na washauri elekezi wa benki hiyo – Aikande Kwayu, Godfrey Telli na Martin Chegere.
Tanzania inaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha tafiti zinatumika katika kuimarisha huduma kwa wananchi.