Habari
TANZANIA NA CHINA KUENDELEA KUSHIRIKIANA KATIKA KUJENGA UCHUMI WA KIMKAKATI
Serikali imeeleza kuwa katika kipindi cha miaka 60 ya ushirikiano wa Tanzania na China, Tanzania imebadili mwelekeo wa sera zake za kiuchumi kutoka utegemezi wa misaada hadi kujenga ushirikiano wa kimkakati wa ujenzi wa miundombinu ya uzalishaji.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb.), aliyeambatana na Katibu Mkuu Dkt.Tausi Kida ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam katika kongamano la miaka 60 ya ushirikiano wa kidiplomasia baina ya mataifa hayo mawili.
Mheshimiwa Prof. Mkumbo amesema kwamba, katika mabadiliko hayo kama ilivyokuwa awali, China ameendelea kuwa mshirika muhimu kwa kuunga mkono ajenda ya Tanzania ya kufanya mapinduzi ya kilimo na viwanda.
Msheshimiwa Waziri wa Nchi, ameeleza kwamba China imekuwa nchi yenye wawekezaji wengi katika sekta ya viwanda, akitolea mfano kiwanda cha Vioo cha Safaya, viwanda vya kuzalisha Malumalu (tiles) na ujenzi wa kongani ya viwanda, Kwara Industrial Park.
Aidha, akiongea kuhusu Kongamano hilo Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo amesema limetoa fursa kuu tatu miongoni mwa nyingine, kuwezesha majadiliano ya maendeleo yanayolenga mkutano ujao wa China-Afrika FOCAC, vilevile, ni fursa ya kufanya tathmini ya ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na China, na kuona fursa zinazoweza kutokea katika siku zijazo.
Kongamano hilo limehusisha mijadala mbalimbali baina ya jumuiya ya wawekezaji wa Tanzania na China na jumuiya za Wanazuoni wa nchi hizo mbili.