Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

TANZANIA NA URUSI KUKUZA USHIRIKIANO WA BIASHARA NA UWEKEZAJI


Tanzania na Shirikisho la Urusi zinakusudia kukuza ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji ili kuimarisha diplomasia ya uchumi baina ya nchi hizo.


Hatua hiyo imebainishwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji Dkt. Tausi Mbaga Kida leo tarehe 28 Oktoba, 2024, jijini Dar es Salaam, wakati wa kikao cha kwanza cha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano wa Biashara na Uchumi kati ya Tanzania na Urusi.
Kikao hicho ni cha ngazi ya juu ya wataalaam ambacho kimejadili na kukubaliana maeneo mahsusi ambayo nchi hizi mbili zitashirikiana katika masuala ya uchumi, biashara na uwekezaji.


Kwa mujibu wa Dkt. Kida, ushirikiao utahusisha maeneo mbalimabli ikiwemo kilimo biashara, madini, utalii, afya na elimu; hatua ambayo itatoa fursa kubwa kwa mataifa haya mawili katika kuinua kiwango cha uchumi na kuboresha maendeleo ya jamii.


Aidha, amebainisha kuwa urafiki baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Shirikisho la Urusi umedumu kwa miongo kadhaa mpaka sasa, hatua ambayo imeziwezesha nchi hizi mbili kujenga mahusiano mazuri ya kijamii na kisiasa.


“Ninauchukulia mkutano huu kuwa ni mwanzo wa kustawisha mahusiano ya kibiashara na kiuchumi kati ya nchi zetu kwa kufungua milango ya kufanya biashara na shughuli nyingine za kiuchumi katika mazingira mazuri na rafiki” Alifafanua Dkt. Kida.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Uwili, Wizara ya Maendeleo ya Kiuchumi ya Shirikisho la Urusi Mhe. Pavel Kalmychek ameishukuru Tanzania kwa kukubali kuongeza wigo wa ushirikiano akisema kuwa itasaidia kuleta maendeleo ya mataifa hayo na jamii kwa ujumla.


Dkt. Kida na Mhe. Kalmychek ni wenyeviti wenza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano wa Biashara na Uchumi kati ya Tanzania na Urusi kwa ngazi ya wataalamu, na leo walikuwa na jukumu kubwa la kuongoza mazungumzo ya kitaalamu kuhusu kuafikiana juu ya ushirikiano.
Mkutano huo utaendelea kesho kwa ngazi ya juu zaidi ambapo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) kwa Upande wa Tanzania na Mhe. Maxim Reshetnikov Waziri wa Urusi anayeshughulikia Maendeleo ya Kiuchumi, watatoa mrejesho kuhusu hatua za makubalino zilizofikiwa.