Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

TANZANIA NI NCHI YA PILI KWA UZALISHAJI WA MVINYO BARANI AFRIKA


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) amesema kwa sasa soko la Mvinyo unaozalishwa Tanzania limekuwa hadi kufika nafasi ya pili kwa ukubwa Afrika baada ya Afrika Kusini hivyo Serikali itahakikisha kiwango cha uzalishaji kinaendelea kukidhi viwango vya kimataifa.

Prof. Mkumbo aliyasema hayo Julai 7, 2024 Jijini Dodoma kwenye hafla ya Uzinduzi wa Bidhaa mpya ya Mvinyo inayotengenezwa na kiwanda cha Alko Vintages.

Mhe. Prof. Mkumbo aliongeza aliongeza kuwa serikali itaendelea kuwaunga mkono wawekezaji ili wakulima wanaozalisha zao hilo waendelee kupata soko la uhakika na kuongeza thamani mazao ya kilimo.

“Kwakweli hiki ambacho mwekezaji wa kiwanda hiki amefanya kinaenda sambamba na ajenda ya Serikali ya uchumi katika suala zima la kuongeza thamani mazao ya kilimo na yeye anatusaidia kuongeza thamani kwenye zao hili la zabibu lakini sambamba na ajenda ya kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi”, alisema Prof. Mkumbo.

Aliongeza kuwa Mvinyo wa Tanzania unakidhi viwango vya kimataifa kutokana na aina tofauti za uzalishaji zinazozalishwa pamoja na wanywaji kuongezeka.

Aidha, alitoa wito kwa wawekezaji kuendelea kutoa ushirikiano kwa serikali na kuwapa sapoti wakulima ili waongeze uzalishaji.

“Mwisho wa siku unahitaji malighafi ili uweze kuzalisha na malighafi hizi zinapatikana shambani, kwa hiyo sisi tunatoa mbegu bora, tunaongeza masuala ya matumizi ya mbolea na kilimo cha umwagiliaji ili wakulima wetu waweze kulima wapate tija kubwa zaidi katika uzalishaji,” aliongeza Prof. Mkumbo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho Bw. Archard Kato amesema mabadiliko ya hali hewa yameathiri upatikanaji wa zabibu hivyo kwa mwaka huu hawategemei kupata malighafi nyingi ikilinganishwa na mwaka uliopita hivyo wataenda kuwasaidia wakulima ili wasiathirike tena na ukame.

“Ili tusiweze kuathirika na hii hali ya hewa hasa suala la mvua kuwa nyingi au wakati mwingine kuwa kidogo ndiyo maana tunataka kusaidia suala la visima ili tatizo la ukame lisiendelee kuwa kikwazo kwa wakulima wetu wa zabibu”, alisema Bw. Kato.

Aliongeza kuwa kwa sasa wataanza kutoa elimu kwa wakulima wa zabibu ili waweze kuhakikisha wanalinda mashamba yao dhidi ya magonjwa na hata magonjwa yakitokea waweze kuyamudu kwa kuwapatia na mikopo ili waweze kukabiliana nayo kwa kununua dawa.