Habari
TANZANIA YAPIGA HATUA KUBWA KATIKA UANZISHWAJI WA STARTUP

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika uanzishwaji wa Startups, huku Serikali ikiendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kukuza uchumi.
Akifungua Kongamano la Wiki ya Startup tarehe 16 Desemba, 2024 Dar es Salaam, Dkt. Biteko ameeleza juhudi za Serikali kupitia kufutwa kwa tozo 374 na kuunganisha taasisi zenye majukumu yanayofanana ili kuondoa urasimu.
Dkt. Biteko amesisitiza ajenda ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwahamasisha vijana kuanzisha Startups na kutumia fursa za mikopo. "Ubunifu wa vijana ndiyo msingi wa uchumi imara," alisema.
Akimkaribisha mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Nyongo, kwa niaba ya Waziri Prof. Kitila Mkumbo, amesema ofisi yake imekuwa mstari wa mbele katika kukuza uwekezaji na kuratibu mipango ya Taifa kama Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Aidha, amebainisha jitihada za kuboresha sera na sheria za uwekezaji ili kusaidia Startups, ikiwemo kurahisisha usajili na kupunguza gharama na muda wa kushughulikia uwekezaji.
Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano, Mhe. Jerry Slaa, ameeleza kuwa Startups ni chanzo kikubwa cha ajira kwa vijana, huku Serikali ikiandaa sera maalum ya kuzikuza.
Tukio hilo limeandaliwa na Startup Tanzania (TSA), ambapo Mwenyekiti wake, Bw. Paul Makanza, amepongeza ushirikiano wa Serikali katika kusaidia sekta hiyo.
Kongamano hili linakusudia kutatua changamoto zinazokwamisha Startups na kusaidia ukuaji wa uchumi wa kidigitali nchini.