Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

TRILIONI 38 ZA PATO LA TAIFA ZINATOKANA NA KILIMO - PROF. MKUMBO


Serikali imesema kuwa sekta ya kilimo ndio injini ya uchumi wa Tanzania, ikichangia zaidi ya robo ya Pato la Taifa. 

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (Mb.), katika Kongamano la Uwekezaji lililofanyika Dodoma leo, Agosti 6, 2024.

Akizungumza katika kongamano hilo, Prof. Mkumbo ameeleza kuwa kilimo si chakula tu, bali ni chanzo kikubwa cha ajira kwa Watanzania milioni 28.6.

Aidha, Mheshimiwa Prof. Mkumbo amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji, teknolojia ya kisasa, na uzalishaji wa mbolea ili kuongeza tija na kuimarisha usalama wa chakula.

"Tanzania imefanya maendeleo makubwa katika sekta ya kilimo katika miaka ya hivi karibuni, na tunalenga kujitosheleza katika mahitaji yetu ya chakula na hata kuwa nchi ya wauzaji," alisema Prof. Mkumbo.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda amepongeza juhudi za Serikali katika kukuza sekta ya kilimo, akisisitiza kuwa mikoa ya Kanda ya Kati ina uwezo mkubwa wa kuchangia katika maendeleo ya taifa.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amewakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali, ikiwemo kilimo, mifugo, uvuvi, utalii, viwanda, na madini.