Habari
TUME YA UTUMISHI WA UMMA YARIDHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI

Tume ya Utumishi wa Umma imeridhishwa na utendaji kazi wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji katika jitihada zake kwenye jukumu la kuvutia na kuhamasisha uwekezaji sambamba na uratibu wa masuala ya mipango nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Mstaafu Mhe. Hamisa H. Kalombola wakati wa kikao cha kufunga ukaguzi (Exit Meeting) uliofanyika katika Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Jijini Dodoma.
Mhe. Jaji Kalombola amebainisha kuwa pamoja na Ofisi hiyo, kuwa imetimiza mwaka mmoja pekee tangu kuundwa kwake mwezi Julai, 2023 na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeweza kutekeleza kwa ufanisi mkubwa majukumu yake kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya Utumishi wa Umma.
“Jukumu la Ofisi hii ni Kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kukuza uchumi wa taifa letu kwa kuwakwamua wananchi kupitia shughuli wanazofanya”.
"Sisi sote tunajenga nyumba moja, naomba muendelee kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili tufikie pale tunapohitaji" ameelekeza Mhe. Jaji Kalombola.