Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

Wadau wa sekta zinazohusika na uwekezaji wametakiwa kutoa maoni yatakayowezesha kupatikana kwa mwongozo bora wa uwekezaji katika maeneo maalumu ya kiuchumi.


Wito huo umetolewa leo Juni 4, jijini Dar es Salaam na Dkt. Tausi Kida, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji alipofungua warsha ya wadau ili kupitia rasimu ya tafiti na mwongozo wa uwekezaji katika maeneo maalum ya kiuchumi.

Katika hotuba yake Dkt. Kida, ametoa msisitizo kwa washiriki wa warsha hiyo kupitia kwa kina changamoto zilizobainishwa katika ripoti hiyo ya awali na mapendekezo ya utatuzi ili kuwa na mipango sahihi ya utekelezaji.

Maelekezo mengine mahususi aliyoyatoa Katibu Mkuu Dkt. Kida yamewataka wadau hao kutathmini hali ya mtawanyiko wa maeneo ya uwekezaji kwa kuegemea zaidi katika mikoa ya karibu na bandari hususani Dar es Salaam na Pwani na kutoa mapendekezo ya kuvutia maeneo kama hayo katika mikoa mingine.

Vile vile, amewataka kutathmini mikakati inayopasa kutekelezwa ili kuvutia uwekezaji kwenye maeneo ya SEZ zaidi ya viwanda ikiwemo kilimo , teknolojia (Technology Parks), utalii, madini na michezo.

Kutathmini sababu za baadhi ya maeneo ya SEZ kukosa wawekezaji na wakati huo huo wawekezaji wakitafuta maeneo yaliyo nje na maeneo ya SEZ.

Kutathmini aina ya vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi iwapo vinaimarisha ushindani kwa kulinganisha na nchi nyingine; na

Kupendekeza namna ya kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi pamoja Halmashauri katika uendelezaji wa Maeneo ya SEZ.

Kongamano hilo limehusisha wadau kutoka wizara za kisekta, wadau wa maendeleo, sekta binafsi na taasisi zinazohusika na maeneo maalumu ya uwekezaji katika maeneo maalumu ya kiuchumi.