Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

WANAHABARI WAPONGEZWA KWA KUTOA TAARIFA KUHUSU DIRA 2050


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, amevipongeza vyombo vya habari kwa mchango mkubwa wa kuhamasisha na kutoa taarifa sahihi juu ya Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 tangu kuzinduliwa kwake na Rais wa Zanzibar, tarehe 11 Desemba 2024.

Akizungumza katika Mkutano wa Wahariri na Wamiliki wa Vyombo vya Habari ambao umefanyika leo tarehe 16 Desemba, 2024, Dar es Salaam, Waziri Mkumbo amesisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kuendelea kutoa taarifa kwa weledi ili kuwafikia wananchi wote na kuwapa taarifa zilizo sahihi na kwa wakati.

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo uliyolenga kupokea maoni ya Wahariri na Wamiliki wa vyombo vya habari, Mhe. Waziri ameeleza kuwa Rasimu ya Dira 2050 inajikita katika misingi thabiti kama vile umoja wa kitaifa, utu, demokrasia, uhuru, na haki.

Aidha, amesisitiza kuwa malengo makubwa ya Dira 2050 ni pamoja na kuondoa umasikini, kuimarisha uchumi unaotegemea uzalishaji wa ndani, na kuifanya Tanzania kuwa kinara wa uzalishaji wa chakula barani Afrika, huku ikilenga kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa 10 wa chakula duniani.

Wanahabari wametakiwa kuendelea kuwa sehemu ya mabadiliko haya makubwa kwa kutoa taarifa zenye kuhamasisha na kuelimisha jamii juu ya mwelekeo wa Taifa kuelekea 2050.