Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

WAZIRI MKUU AZITAKA MAMLAKA ZA UTHIBITI KUFANYA KAZI KWA PAMOJA


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), ameziagiza mamlaka ya uthibiti na ukaguzi kufanya shughuli zao kwa pamoja ili kuondoa urasimu na usumbufu kwa wawekezaji na wafanyabiashara wanaowekeza nchini.

Mhe. Majaliwa ametoa kauli hiyo Septemba 11, 2024 katika ukumbi wa Mlimani jijini Dar es salaam aliposhiriki hafla ya mwaka mmoja wa kuanzishwa kwa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji iliyoambatana na uzinduzi wa Taarifa za Maboresho ya Mazingira ya Uwekezaji na Biashara na Nyenzo za Usimamizi wa Uwekezaji Nchini.

"Taarifa na nyenzo zinazozinduliwa leo zina umuhimu mkubwa katika kuimarisha mazingira ya uwekezaji na biashara hapa nchini lakini pia zinatoa muongozo, kuboresha taratibu na kuongeza ufanisi" amesema.

Akizungumza kuhusu uzinduzi huo Mhe. Waziri Mkuu amesema, nyenzo hizo zitasaidia katika kupima maendeleo ya Nchi Kwa kuonesha changamoto tunazopitia, lakini pia zinatoa muelekeo sahihi wa uwekezaji na mazingira rafiki ya uwekezaji yenye ushindani.

Katika hotuba yake Mhe. Waziri Mkuu amezitaja taasisi za mfano kama Jeshi la zimamoto, OSHA na Shirika la viwango nchini (TBS) na kusema kuwa  hatua ya kufanya kazi kwa pamoja zitapunguza usumbufu na kero kwa wafanyabiashara kwa kutumia muda mrefu kufuatilia na kutekeleza taratibu za kiserikali.

Aidha ameziagiza taasisi hizo na Mamlaka za serikali za mitaa kuharakisha marekebisho ya taratibu na sheria mbalimbali ambazo zitachangia urahisi wa kufanya biashara nchini Tanzania akitaka sheria hizo ziwezeshe mazingira bora ya uwekezaji kwa kila eneo.